
|
Johanseni Felisiani: JE, WAJUA KUHUSU WOKOVU?
Jikusanyeni mje na kukaribia pamoja enyi wa mataifa mliookoka, hawana maarifa wale wauchukuao mti wao wa sanamu ya kuchonga wamwombao Mungu asiyeweza kuokoa. (Isa 45:20) Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia, maana mimi ni Mungu; hapana mwingine. (Isa 45: 20)
I. Je, WOKOVU NI NINI?
Kuna mitazamo na maoni mbalimbali kuhusu jambo hili Wokovu. Wengine hufikiri kwamba kuokoka ni kubatizwa. Wenginne hufikiri kuwa wokovu ni kujiunga na dini fulani. Wengine hufikiri kuwa kuokoka ni kuacha kunywa pombe, kuvuta sigara n.k. Bila shaka na wewe unao mtazamo wako kuhusu jambo hili la wokovu.
Je ni nini maana kamili kuhusu jambo hili? Hebu fuatana nami katika maelezo yafuatayo. Awali ya yote napenda kueleza kuhusu tofauti iliyopo kati ya Dini na Wokovu.
Dini ni njia za mwanadamu kumtafuta Mungu, ndiyo maana kuna dini nyingi, zingine za kweli na nyingine zisizo za kweli. Kila mtu anayo dini hata wachawi, walevi, makahaba, wote wana dini zao.
Wokovu ni njia ya pekee ya Mungu ya kumtafuta Mwanadamu.
II. KWA NINI MUNGU ANAMTAFUTA MWANADAMU?
Neno kutafuta linaonesha kuwa kuna kitu kimepotea, hivyo kinatafutwa ili kirudishwe mahali pake. Yesu anasema: Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. (Lk 19:10) Je kilichopotea ni nini? Bila shaka ni Mwanadamu.
Mungu alimuumba mwanadamu akiwa mkamilifu na mtakatifu, maana aliumbwa kwa mfano wa Mungu bila kosa lolote.
Pia alikuwa na ushirika mzuri na Mungu. Katika Bustani nzuri ya Edeni, Mungu alimpa maagizo yaliyompasa kufuata na kuishi kwayo. (Mwa 2:16–17)
Lakini mwanadamu alidanganywa na shetani akaasi maagizo ya Mungu, hivyo akapotea kutoka katika njia ya Mungu na utakatifu wake. Kutokana na dhambi hiyo mwanadamu amekuwa mateka wa shetani na mtumwa wa dhambi. (Yn 8:34)
Hivyo akili ya mwanadamu na ufahamu wake juu ya Mungu wa kweli ilipotea, ndiyo maana leo hii kuna watu wanaoabudu viumbe walivyopewa na Mungu kuvitawala, kama vile ng’ombe, mawe, miti, jua, mwezi, pesa, n.k. (Mwa 1:26–27; Rum 1:21–30) Haya yote ni matokeo ya uasi wa mwanadamu.
Mateka au mtumwa hana hiari ya kuamua chochote anachotaka, badala yake hulazimishwa kufanya vyovyote kulingana na matakwa ya bwana wake. Hivyo mwanadamu kwa sababu ni mateka wa shetani hulazimishwa kufanya mambo maovu asiyotaka kufanya, kama vile ubakaji, uuaji, uzinzi, ukahaba wizi, kutumia madawa ya kulevya, kuabudu sanamu na uchawi.
Ndiyo maana Mungu anamtafuta mwanadamu. Yawezekana wewe ndugu yangu ni mmoja wa watu wanaoishi katika utumwa huo, hata inawezekana umejaribu kuacha mambo hayo lakini bado umeshindwa.
Yawezekana umejaribu kusali, kwenda Kanisani au Msikitini kutafuta msaada lakini imeshindikana. Ni kweli huwezi kupata msaada kwa njia yoyote isipokuwa kwa MWOKOZI TU.
III. MWOKOZI NI NANI?
Zipo dini nyingi duniani na wapo waanzilishi wengi wa dini hizo laMkini yupo mwokozi mmoja tu. Huyo anaweza kusamehe dhambi zote, Biblia inasema katika Injili ya Mathayo. Naye atazaa mwana nawe utamwita jina lake Yesu maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. (MT 1:21)
Ni Yesu tu anayeweza kukutoa katika utumwa wa dhambi na kukupa uhuru wa kweli. Katika kitabu cha Matendo ya Mitume maneno ya Mungu yanasema: Huyo manabii wote humshuhudia ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi. (Mdo 10:43)
Yesu alikufa msalabani kwa ajili yako ili aweze kukuokoa, damu yake iliyomwagika inatosha kusafisha dhambi zako zote. Yeye anakutafuta, anakuita akisema: Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Mt 11:28)
IV. UFANYEJE ILI KUPATA WOKOVU?
1. Kubali kwamba wewe ni mwenye dhambi unayestahili hukumu ya Mungu, maana neno la Mungu lasema: Mshahara wa dhambi ni mauti. (Rumi 6:23)
Elewa ya kwamba Mungu anafahamu mambo yako yote na huwezi kujiokoa mwenyewe.
2. Kumbuka ya kwamba Mungu anakupenda. Alimtoa Yesu afe msalabani kwa ajili yako na dhambi zako, (Rum5:8; Yn 3:16)
3. Mkaribishe Yesu ndani ya moyo wako, yeye anasema: Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akisikia sauti yangu, na kufungua mlango, nitaingia kwake. (Ufu 3:20)
4. Tubu dhambi zako sasa kisha uamue kuziacha kabisa, Bwana yuko tayari kukusamehe yeye anasema: Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako. (Isa 43:25) Waweza kufanya uamuzi huu hata hivi sasa unavyoendelea kusoma maneno haya, maana Bwana yupo pamoja nawe hapo hapo ulipo.
5. Kubali kupokea kwa Imani msamaha wa dhambi zako kwani hata kama zilikuwa nyingi kiasi gani, nazo zimefutwa zote, kumbuka Neno la Mungu linasema: Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito, na dhambi zako kama wingu; unirudie; maana nimekukomboa. (Isa 44:22) Yesu yu tayari kukutoa katika utumwa wa dhambi na hukumu ya Mungu.
V. MATOKEO YA WOKOVU NI NINI?
a. Kuhesabiwa haki
Baada ya toba yako ya kweli juu ya dhambi zako na Imani katika Kristo Yesu, umehesabiwa haki mbele za Mungu. Neno la Mungu lasema: Lakini sasa haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na Torati na manabii ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kirsto kwa wote waaminio. (Rum 3:21–22)
b. Amani
Tena neno la Mungu lasema: Tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. (Rum 5:1)
c. Kuwa mwana wa Mungu.
Baada ya kumpokea Yesa na kazi yake ya wokovu, sasa wewe ni mtoto wa Mungu. Biblia inasema: Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu. (Yn 1:12.) Wewe si mtumwa tena. (Rum 8:15–16) Tafuta ushirika na watoto wa Mungu waliookoka kama wewe, jitahidi kutunza usafi na utakatifu ulioupokea, maana wewe sasa ni kiumbe kipya. (2 Kor 5:17)
Mungu akubariki sana! Ukiwa na maswali waweza kuwasiliana nami kwa njia hii.
Mchungaji Johanseni Felisiani Iringa Tanzania
|