Teuvo Kopra
www.teuvokopra.fi
Suomi            Tanzania

Teuvo Kopra:

MAJITU katika Agano la Kale

Hawa majitu kama Goliathi na wengine waliojulikana katika Agano la Kale walikuwa kina nani?

Biblia inatuambia kwamba Daudi alimshinda Goliathi.

Goliathi alikuwa jitu lenye urefu wa zaidi ya mita tatu.

Kwa kuongezea Biblia inatutajia majitu mengine kwa majina, kama Ahimani, Sheshai, Talmai, Safu, Lahmi, Ishi-benobu na wengine pia.

Hawa majitu walitoka wapi? Walielewaje Israeli? Waliwaza nini juu ya Israeli?

Na Mungu aliwaelewaje?

Mungu aliwaza nini juu yao?

Mbona siku hizi hatuna majitu?

Au labda bado wako duniani?

Kuna majitu mengi yanaendelea kufanya kazi siku hizi pia.

MAJITU

Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. (MWA 6:1-4)

Biblia ya Kiswahili inatumia jina Wanefili. Wanefili maana yake ni majitu. Majitu ni sawasawa na Wanefili.

Tulisoma mambo yaliyotokea kabla ya Gharika. Majitu yaani wanefili walikuwepo kabla na baada ya Gharika. Majitu yale yalioishi kabla ya Gharika yalifia majini, wakati wa Nuhu. Lakini mambo ya majitu hayakuishia wakati wa Gharika, kwani yalizaliwa tena baada ya Gharika pia.

Tukianza kutaja miaka katika Biblia tangu kuzaliwa kwa Adamu tunaona kwamba Gharika ilitokea mwaka wa elfu moja mia sita hamsini na sita (1656) baada ya kuzaliwa kwa Adamu. Wakati huo watu walikuwepo mamilioni. Katika hali nzuri umri ya watu ulikuwa mara kumi zaidi ya siku hizi. Hivyo kuongezeka kwao kulitokea kwa haraka zaidi.

Sasa tunapochunguza swala la majitu, ni vizuri kukumbuke kwamba Biblia inasema: Hatujui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua. (1KOR 8:2) Na Biblia inasema pia: Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; (1KOR 13:9)

Labda unafikiri kwamba hakuna umuhimu kuchunguza na kuongea kuhusu mambo ya majitu, mambo ya wanefili. Mimi ninakuuliza kwamba kwenye Biblia kuna jambo ambalo halina umuhimu wa kuchunguza? Mambo ya maajabu yote yaliyoko kwenye Biblia ni vipawa kutoka kwa Mungu na ni vizuri tuyachunguze kwa unyenyekevu, na shukrani na tuyapokee. Ingawa tuna upungufu katika kujua Neno la Mungu, hata hivyo kuna umuhimu wa kuchunguza na kutafuta maarifa tukisaidiwa na Roho Mtakatifu wa Mungu. Roho Mtakatifu asipotufunulia maandiko hatuelewi Biblia. Hivyo tunategemea kabisa Roho Mtakatifu atusaidie katika kufunua maandiko.

Biblia inatupa majina ya majitu kumi hivi. Kwa kuongezea wamekuwepo uzao wa majitu Waanaki na Warefai. Zamani Waamoni waliwaita Warefai kwa jina Wazamzumi. (KUM 2:20) Kwanza tunataka kujua:

 

UKUBWA wa MAJITU

Kwani aliyesalia katika mabaki ya Warefai ni Ogu pekee, mfalme wa Bashani; tazama, kitanda chake kilikuwa kitanda cha chuma; kitanda hicho, je! hakiko Raba kwa wana wa Amoni? urefu wake ulikuwa ni mikono kenda, na upana wake mikono minne, kwa mfano wa mkono wa mtu. (KUM 3:11)

Mkono ni sawa sawa na dhiraa. Urefu wa mkono moja, yaani dhiraa moja ni karibu na nusu mita. Mikono kenda, yaani tisa ni kama mita nne. Mikono nne ni karibu na mita mbili.

Hatuelezwi ukubwa wa Ogu, lakini urefu wa kitanda chake ulikuwa ni mikono tisa, yaani mita nne, na upana wa kitanda ulikuwa ni mikono minne, yaani karibu na mita mbili. Kuna vitanda vichache pamoja. Swala lilimhusu mfalme wa Warefai Ogu. Ni lazima alikuwa ni mtu mwenye mwili mkubwa kwa sababu alihitaji kitanda kikubwa sana.

Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. (1SAM 17:4)

Urefu wake Goliathi ulikuwa kama mita tatu. Mguu wake ulikuwa mkubwa ingemlazimu kuvaa viatu viwili. Viatu viwili kila mguu. Wakati wa kwenda kulala vitanda viwe vikubwa viwili au vitatu vimefuatana. Mstari unaofuatia unahusu silaha zake.

Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ili darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. (1SAM 17:5)

Na ..amevaa darii ya shaba; ... ulikuwa kilo themanini ambao ni nzito zaidi ya uzito wangu. Tunagundua kwamba majitu walikuwa wakubwa na wenye nguvu sana.

NIA ya MAJITU

Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. (1SAM 17:8)

Goliathi alisema kwamba Waisraeli ni watumishi wa Sauli. Roho wa Mungu ilimtoka Sauli. (1SAM 16:14) Hivyo ilikuwa vizuri kwa Goliathi kudhihaki. Ukweli ni kwamba Waisraeli walikuwa watumishi wa Mungu, siyo watumishi wa Sauli tu. Ilitakiwa iwe hivyo.

Katika mstari wa 43 Goliathi aliapa na kulaani kwa jina la miungu yake. Yeye alikuwa amejitoa kuabudu sanamu na alimlaani Mungu wa Israeli. Yesu alisema: Kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. (MT 12:34) Moyoni mwake wa Goliathi ulijazwa na mambo mabaya. Jitu yeye alidhihaki, alisema uongo, aliapa kwa miungu yake, alijivuna, alikuwa hayawani na katili. Ni mambo yasiyofanana na yale Mungu anavyotaka tuwe.

Tusome sehemu fupi kuhusu historia ya Israeli. Hii ni wakati wana Waisraeli walitoka utumwani wa Misri kuelekea kwenye nchi ya ahadi.

Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tupeleke watu mbele yetu, ili watupelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji mtakayoifikia. (KUM 1:22)

Tungesoma zaidi Biblia (KUM 9:23,24) tungegundua kwamba Mungu alitaka kuwatoa wakati ule na kuwapeleka katika nchi ya ahadi lakini wale watu walileta fujo walikataa. Hivyo waliwaomba wapelelezi na Mungu akasema: “Endeni mkapeleleze. Kwa sababu hamna imani mioyoni mwenu na katika mawazo yenu, piteni katika njia ambayo ni mavuno ya kutokuamini kwenu. Endeni mkaangalie kwani hamwamini yale niliyowaambia."

Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sinai hata Rehobu, mpaka kuingia Hamathi. Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri. (HES 13:21,22)

Hapa tunawaona majitu. Katika uzao wa Anaki wanapatikana Ahimani, Sheshai na Talmai. Wale wapelelezi walikutana na wale majitu ambao Kalebu aliwafukuza baada ya miaka sitini. Waliongea pamoja na majitu. Baada ya hapo walirejea tena kwenye kambi ya Waisraeli kwa Musa. Halafu waliwaeleza kuhusu safari yao.

Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.(HES 13:28,32)

Walikutana na majitu watatu tu. Hawa walibaki sana kwenye mawazo yao baadaye waliona watu wote kuwa na wakubwa wale.

Kisha, huko tuliwaona kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi. (HES 13:33)

Wanefili maana yake ni majitu. Wapelelezi walijiona udogo wao, walijiona kuwa kama mapanzi. Halafu walisema: "nao ndivyo walivyotuona sisi." Wapelelezi walijua kwamba majitu wamewaona kama mapanzi. Wao walijuaje? Ni kwa sababu majitu waliwaita: "Ninyi mapanzi."

Wapelelezi wawili kati ya wale kumi na mbili Kalebu na Yoshua walikuwa na roho ingine. Walikuwa na roho ya kuamini. Wale wengine walikuwa na roho kama wale waliobaki kambini, yaani roho ya kutokuamini. Yoshua na Kalebu walisema katika sura ya kumi na nne, mstari wa tisa, kwamba: wao ni chakula kwetu. Wengine wanawaonaje majitu, wengine kama chakula?

Neno hilo wanaweza kuliona kwa njia tofauti? Kutokuamini inawaangalia wanaonekana, imani inaangalia yanayowezekana kwa Mungu! Majitu hawa waliwadhihaki watu wa Mungu na watasababisha watu wakae katika kutokuamini na hofu, na hivi safari yao ilichukua miaka arobaini, kabla hawajafika nchi ya Kanani. Majitu hawakuweza kuzuia kufika kwao, ila walifanya safari ya wana wa Israeli iende pole pole zaidi. Kutokuamini inajaribu kufanya hivi pia katika maisha yetu kwamba tusingeweza kukua upesi na kusafiri upesi bali pole pole tu.

NIA YA MUNGU KUHUSU MAJITU

Sikiliza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita wewe, miji mikubwa iliyojengwa kuta hata mbinguni, watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki? Basi jua siku hii ya leo kuwa Bwana, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwa poteza upesi, kama alivyokuambia Bwana. (KUM 9:1-3)

Mungu alikubali kuwa kama moto uteketezao, ata waangamiza na kuwaangusha majitu. Mungu alisema: watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki. Kwa msaada wa Mungu Waisraeli waliwafukuza na kuwapoteza. Mungu aliwachukia majitu.

Vile vile kama Bwana alivyomwamuru Musa mtumishi wake, ndivyo Musa alivyomwamuru Yoshua; naye Yoshua akafanya vivyo; hakukosa kufanya neno lo lote katika hayo yote Bwana aliyomwamuru Musa. Wakati huo Yoshua akaenda na kuwakatilia mbali hao Waanaki watoke nchi ya vilima, kutoka Hebroni, na kutoka Debiri, na kutoka Anabu, na kutoka katika nchi yote ya vilima vilima ya Yuda, na kutoka katika nchi yote ya vilima vilima ya Israeli; Yoshua akawaangamiza kabisa na miji yao. Hawakusalia Waanaki hata mmoja katika nchi ya wana wa Israeli isipokuwa katika Gaza, na katika Gathi, na katika Ashdodi walisalia. (YOS 11:15, 21, 22)

Waanaki ni uzao wa majitu. Wakati wa kuwaangamiza majitu Yoshua alitekeleza agizo hilo Mungu aliyomwagiza Musa. Na hivi majitu walibaki nje ya maeneo ya Waisraeli.

Kisha alimpa huyo Kalebu mwana wa Yefune sehemu kati ya wana wa Yuda, kama Bwana alivyomwamuru Yoshua, maana ni Kiriath-arba, ni huyo Arba aliyekuwa babaye Anaki (Huo ndio Hebroni). Huyo Kalebu aliwafukuza watoke hapo hao wana watatu wa Anaki, nao ni Sheshai, na Ahimani, na Talmai, wana wa Anaki. (YOS 15:13, 14)

Arba na Anaki walikuwa majitu kama vile vile Sheshai, na Ahimani, na Talmai, wana wa Anaki. Kalebu alikutana na aliyowafahamu zamani. Kalebu amesema kwamba majitu ni chakula tu. Aliwafukuza mbali. Daudi aliambiwa na Biblia, kwamba katika yote alitimiza matakwa ya Mungu. (MDO 13:22) Alifanya mapenzi ya Mungu hata kuhusu majitu.

Tunasoma tena kuhusu Daudi na huyu Goliathi wa Gathi. Goliathi alikuwa jitu, kama unavyokumbuka. Urefu wake ulikuwa mita tatu.

Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. Hivyo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia. (1SAM 17:48-51)

Ndivyo alivyoenenda Daudi aliyependeza moyo wa Mungu. Daudi alimwua jitu Goliathi. Hata watumishi wake pia.

Basi kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Israeli; Daudi akashuka mpaka Gobu, na watumishi wake pamoja naye, akapigana na Wafilisti; naye Daudi akaishiwa na nguvu. Naye Ishi-benobu, aliyekuwa mmojawapo wa Waferai, ambaye uzito wa mkuki wake ulikuwa shekeli mia tatu za shaba kwa uzani, naye amejifungia upanga mpya, alijaribu kumwua Daudi. Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akamsaidia, akampiga Mfilisti, akamwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, wakasema, Wewe hutatoka tena pamoja nasi kwenda vitani, usije ukaizima taa ya Israeli. Ikawa baada ya hayo, kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; ndipo Sibekai, Mhushathi, alipomwua Safu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai. Kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; na Elhanani, mwana wa Yairi, Mbethlehemi, alimwua Goliathi, Mgiti, ambaye mti wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumaji. Kulikuwa na vita tena huko Gathi; ambako kulikuwa na mtu mrefu sana, mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake ishirini na vinne; yeye naye alizaliwa kwa Mrefai. Naye huyo alipowatukana Israeli, ndipo Yonathani, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akamwua. Hao wanne walizaliwa kwake huyo Mrefai wa Gahti; wakaanguka kwa mkono wa Daudi, na kwa mikono ya watumishi wake. (2SAM 21:15-22)

Warefai walikuwa kabila la majitu. Tulisoma majina ya majitu: Ishi-benobu, Safu wa Warefai, Goliathi. Katika mistari hii tunaona tabia za hao majitu na jinsi Mungu alivyowafikiria. Ishi-benobu alinuia kumwua Daudi aliyekuwa amechoka, lakini Abishai, mtoto wa dada yake Daudi alimwua yule jitu na hivyo akaokoa maisha ya mjomba wake.

Sibekai alimwua Safu. (1NYA 20:4). Elhanani alimwua Goliathi wa Gathi, aliyeitwa kwa jina jingine, Lahmi katika kitabu cha NYAKATI. (1NYA 20:5). Yeye alikuwa amechukua jina la nduguye Goliathi, aliyeuawa na Daudi. Daudi alimwua Goliathi akiwa kijana kwa jiwe na kombeo. (1SAM 17). Huyu jitu mwenye vidole vya mguuni sita na vidole vya mkononi sita aliuawa na Yonathani kijana wa ndugu yake Daudi. Benaya, mtu hodari wa Daudi, katika vita pia alikuwepo katika kuwaangamiza majitu.

Tena, Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari, wa Kabseeli, aliyekuwa amefanya mambo makuu, ndiye aliyewaua simba wakali wawili wa Moabu; pia akashuka, akamwua simba katikati ya shimo wakati wa theluthi. Huyo akamwua Mmisri, mtu mrefu sana, aliyekuwa wa dhiraa tano urefu wake; na yule Mmisri alikuwa na mkuki kama mti wa mfumaji mkononi; lakini yeye akamshukia na gongo, akamnyakulia Mmisri mkuki mkononi, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe. Mambo hayo ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, akawa na jina kati ya wale mashujaa watatu. (1NYA 11:22-24)

Jitu wa Misri lilikuwa na urefu wa mita mbili na nusu. Sisi tumegundua kwamba mkono wa Mungu ni kinyume cha majitu. Kwa kuwaangamiza majitu Mungu alimtumia Daudi na mashujaa wake wa vita. Hao waliwaangamiza hata wale majitu waliokuwa nje ya makazi ya Waisraeli, waliokuwa wameishi huko kuanzia wakati wa Kalebu na Yoshua, yaani kama miaka mia nne.

MUHTASARI

Nia ya majitu: Waliwapinga walio wa Mungu, kazi ya Mungu, mipango na matakwa yake. Walimwaibisha Mungu, walidhihaki na kutukana watumishi wa Mungu. Mawazo ya Mungu juu ya majitu: Mkono wake daima ulikuwa kinyume chao hivyo kuwaangamiza duniani.

HAWA MAJITU WALIKUWA KINA NANI?

Biblia haitupi maelezo ya moja kwa moja ya wazi na ya kutupisha. Uamuzi wetu inabakia chini ya tafsiri yetu hafifu. Mungu kwa njia ya Biblia haridhishi utafiti wetu. Biblia inatueleza wazi na kwa kurudia yale yote yaliyomuhimu kwa ajili ya wokovu kwa binadamu, kukua kiroho na ili tujifunze kumjua huyu Mungu wa upendo. Lakini hairidhishi upekuzi wetu.

.... wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. (MWA 6:2,4)

Wanefili ni sawasawa na majitu. Tulisoma: wana wa Mungu waliwaona hao binti ... Wana wa Mungu - walikuwa kina nani waliokua baba ya majitu? Yesu ni mwana pekee wa Mungu. (YN 3:16). Wanaomwamini Yesu wanaitwa wana wa Mungu. (1YOH 3:1). Hatusomi, lakini wana wa Mungu wanatajwa pia katika kitabu cha Ayubu. (AYU 1:6).

Labda hao walikuwa malaika, au viumbe vingine kutoka mbinguni. Wachunguzi wa Biblia wamekubaliana kwamba wale wana wa Mungu waliotajwa katika MWANZO ambao baadaye wakawa baba ya majitu ni wale malaika wa uovu, malaika walioanguka, pepo waliochukua miili ya wanadamu. Biblia inasema kwamba malaika wanafanana na vijana.

Malaika wenye nguvu sana.

Inawezekana: wana wa Mungu walikuwa malaika walioanguka, waliochukua miili ya binadamu. Shetani anaweza kubadili mavazi. Alikuwa Bustani ya Edeni katika mwili wa nyoka. Hawa wenye miili ya binadamu walioa na wanadamu. Majitu walizaliwa.

Inawezekana hawa wanawake walioolewa na wana wa Mungu walijitoa mioyo yao yote katika utawala mbaya. Tulisoma MWANZO, sura ya sita, mstari wa pili, kwamba: wana wa Mungu ... wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. Walimchukua yeye, yule alijitoa kwake kuabudu dhambi na shetani. Na hivi majitu walizaliwa.

Sasa tunaweza kuuliza, Je! hawa majitu waliozaliwa walikuwa wanadamu au mapepo? Baba ya majitu alikuwa pepo, lakini mama yao alikuwa mwanadamu.

Tunakumbuka Yesu alipozaliwa kwa Roho Mtakatifu na Mariamu. Yesu alikuwa Mungu, na pia mwanadamu. Mwili wa nje wa Yesu ulikuwa na sura ya mtu. Uungu ulikuwa rohoni. Yesu alikuwa mtu kwa nje, lakini Mungu ndani yake. Inawezekana majitu walikuwa watu wenye miili mikubwa, lakini rohoni walikuwa mapepo. Nje majitu ndani mapepo.

KWA NINI SHETANI ALILETA MAJITU DUNIANI?

Shetani anajua kwamba duniani yuko kwa muda, baadaye atapata hukumu ya milele Jehanamu. Ndipo ameamua: "Mimi siendi Jehanamu, iliyotengenezwa kwa ajili yangu, bali nitavuruga mipango ya Mungu, ili yasitimie. Hivyo hakuna hukumu ya mwisho wala sitaingia Jehanamu." Shetani alifikiri hivi. Ndipo alianza kuvuruga. Kwanza alimwangusha mwanadamu dhambini huko Bustani ya Edeni.

Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. (MWA 2:9)

Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima. (MWA 3:22-24)

Adamu na Hawa walifanya dhambi na Mungu aliwafukuza toka Bustani ya Edeni. Shetani alitaka mwanadamu ale kutoka mti wa uzima. Kama mwanadamu kwa vishawishi vya Shetani ale kutoka mti wa uzima, mwanadamu angeishi milele. Na kama mtu angeishi milele, hakuna hukumu ya mwisho.

Bali Mungu aliwahi kumfukuza mwanadamu atoke karibu na mti wa uzima. Kama Mungu asingewahi, kifo haingekuwepo, wala hukumu ya mwisho, hata mwisho wa dunia na Jehanamu. Shetani angeepuka kuingia Jehanamu. Mwanadamu alikatazwa kula matunda ya mti wa uzima, hiyo kifo kikaja kwake.

Shetani alishindwa na mipango yake alishindwa kuvuruga mipango ya Mungu.

Bwana akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. (MWA 3:14,15)

Mungu alimwambia Shetani, kwamba mwanamke ... atakuponda kichwa. Biblia inafananisha sehemu nyingi taifa la Israeli kama mke wa Mungu. (ISA 54:5,6, YER 3:6,12)

Mateso ya Shetani juu ya Israeli imeanza tangu awali na inazidi kupata nguvu. Shetani aligundua: "Kadri ya ahadi ya Mungu kwamba uzao wa mwanamke itaponda kichwa changu. Uzao wa mwanamke ni Masihi. Yaani mimi nitatupwa Jehanamu. Hivyo nachafua wanadamu, wote asitokee uzao safi wa mwanamke atakaye timiza ahadi ya Mungu juu ya Masihi." Shetani alifikiri hivi. Hivyo wale malaika wa Shetani walichukua mwili wa mwanadamu, wakaoa mabinti wa wanadamu hivyo majitu walizaliwa. Hao walikuwa uzao wa Shetani tulio soma juu yao katika Mwanzo, sura ya tatu, mstari wa kumi na tano. Hawa hawakuwa wanadamu wasafi bali walikuwa mchanganyiko na Shetani.

Tunaposoma Biblia tunagundua kwamba majitu hawa hawakuchukia taifa lingine bali Israeli tu. Waliishi vizuri na Wafilisti na wengine. Uzao wa mwanamke lazima ungekuwa Mwisraeli. Angechafua taifa hili peke yake, kwa sababu Masihi atakuja kutoka taifa la Israeli. Majitu walipata na watu wengine kuwasaidia kazi yake. Waliinuka juu ya Israeli, kama tunavyoona hata leo.

Mariamu, mwanamke wa Mwisraeli alimzaa Masihi. Mariamu alikuwa mwanadamu kamili. Unabii ulisema kwamba Yesu angezaliwa kutoka uzao wa Daudi. Shetani alitumia majitu, watumishi wake na alimsumbua Daudi zaidi kuliko watu wengine. Shetani alijua: Daudi angaliuawa, Masihi asingalizaa katika uzao wa Daudi.

Kabla ya hapo Shetani na majitu walijaribu kuzuia Waisraeli wasingie nchi yao. Walishindwa ila kusogeza kuja kwao miaka arobaini. Na baadaye Shetani alijaribu kuua mbegu ya mwanamke, yaani Yesu mara baada ya kuzaliwa. Tunakumbuka mauaji ya watoto Bethlehemu baada ya Yesu kuzaliwa. (MT 2). Na tena Shetani alishindwa. Yesu aliposulubiwa, Shetani aliwaza ameshinda lakini kwa kifo chake Yesu alipata ushindi mkubwa. Yesu aliponda kichwa cha nyoka.

Hata siku hizi Shetani anajaribu kuiangamiza Israeli. Shetani ametumia mambo tofauti kwa kuiangamiza Israeli. Siku zijazo mashambulizi ya Shetani juu ya Israeli zitaendelea, na kuongezeka, lakini atashindwa. Ahadi za Mungu zijazo kwa sehemu kubwa zinawahusu Waisraeli. Iwapo Israeli itaangamizwa ahadi za Mungu hazitatimia. Hukumu ya mwisho isingetokea, hakuna Jehanamu. Shetani angefurahia ushindi na angekuwa huru na hukumu ya Jehanamu.

Siku hizi Shetani anapinga mipango ya Mungu kwa nguvu na mamlaka yake yote. Mapambano hayana matumaini. Swala ni juu ya hukumu ya mwisho Jehanamu, na Shetani haendi huko kwa hiari. Anajua huko kuna nini. Wasioamini wangechukua mfano toka Shetani, kuikimbia Jehanamu. Mwanadamu ana uwezekano wa kuokoka, lakini Shetani hana.

Tunagundua hapa tunaposoma Biblia, kwamba kila mara Mungu ameshinda na Shetani ni yule anayeshindwa. Ingawa sehemu zingine Shetani anafaulu na tunajisikia tunashindwa na wanyonge, lakini ni vizuri kujua kwamba vita vyote tutashinda na tutashinda hakika.

JE, MAJITU BADO WANAWEZA KUZALIWA?

Je, wale mashetani bado wanaweza kuchukua mwili wa mwanadamu na kuoa wanawake? Je, majitu wanaweza kuzaliwa, nusu shetani, na nusu mtu?

Hapana!

Shetani alijaribu kukataa kwamba Masihi hawezi kuzaliwa. Mariamu amezaa. Masihi amekuja na kupata ushindi. Watu wote wamenunuliwa Golgotha kwa Mungu. Mamlaka ya Shetani imepondwa na imewekwa mipaka. Mungu anatoa amri na ruhusa sehemu ambazo shetani anaruhusiwa kufanya kazi zake.

Baadaye Shetani atafungwa miaka elfu moja. Ni wakati mzuri wa utawala wa Mungu hapa duniani. Baadaye Shetani atapewa likizo kidogo kisha baadaye atatupwa Jehanamu milele. (UFU 20). Kama Shetani anazuia ahadi za Mungu hazitimii. Shetani hataki kuenda jela wala Jehanamu.

Watu wote wana nafasi ya kuokoka. Hata mwenye dhambi zaidi! Shetani hata kwa kutumia majeshi ya majitu hawezi kuzui safari ya mwenye dhambi kuja kwa Yesu. Shetani anapinga kuokoka na anafanya vita vikali. Lakini majitu hawapo hapa bali mitindo ya Shetani ni mingine siku hizi lakini roho ni ili ile. Mtu anapomgeukia Yesu, baadaye anarithi mbingu. Ukijiachia kwa Shetani utashindwa milele na ya baadaye ni mabaya. Wa Mungu wana uajayo mazuri. Walio wa Shetani watapata mabaya.

MAJITU ya SIKU HIZI

Ingawa siku hizi hatuna majitu wa mita tatu, Shetani akiwa yule yule, anaendeleza kuonekana kama jitu. Majitu ya siku hizi majina yao ni tofauti na ya zamani.

Katika maisha ya wengi HOFU ni kama jitu kubwa. Kuna hofu ya mambo yajayo, hofu ya magonjwa, hofu ya kutokufanikiwa, hofu ya kukataliwa na kadhalika. Siku zingine hofu ya namna hii inamtishia na kumsumbua mwenye hofu na kujifanya kama majitu. Ndio kwa sababu kuna roho ile ile. Yesu alisema mara nyingi: Usiogope!

Majitu machache yanatembea tembea yakisababisha uharibifu. Kama WIVU, HASIRA, KUTOKUSAMEHE na PESA. Tujihadhari na hawa. Tunayashinda kwa imani.

Mara nyingi jitu linakuja kusema na walioamini mambo ya kutokuamini na upotovu. Jitu la UONGO linasema: "wewe huendi mbinguni. Kwa mwendo wa udhaifu hivi si rahisi kuingia mbinguni. Mungu hasikilizi maombi yako manyonge. Hata hupati jibu." Hivi jitu la Uongo linasema.

Ukibaki kuwasikiliza majitu haya utapotea amani na imani. Kazi ya yao majitu ni kutoa jina lako katika kitabu cha uzima. Au kufanya safari yako iwe ngumu. Kumbuka kwamba Yesu hatafuti wale wanaopambana kwa kufaulu bali anatafuta wale wanaomfuata kwa uaminifu.

Waaminio wanawashinda majitu hata siku ya leo. Ingawa majitu ya siku hizi bado yanalaani na kupinga mipango ya Mungu na kutulisha, wafuasi wa Yesu, tukumbuke kwamba Mungu ni upande wetu. Yeye ni mkubwa zaidi ya majitu na anatupigania.

Majitu yapo hata siku ya leo. Miili yao mikubwa na sauti zao kubwa haziwezi kuzuia msafara wa ushindi kuelekea mbinguni. Yesu anakusaidia kupambana na majitu yanayokusumbua. Mtu anayetafuta wokovu na msamaha wa dhambi, asingeamini uongo wa shetani ingawa yanaonekana kama majitu mbele yake.

Kumbuka kwamba Yesu anaweza kusamehe dhambi na anataka kuokoa watu wote.

Uniandike:
teuvo.kopra@gmail.com

(Copyright Teuvo Kopra)

   

WebDesign Miia Metsola