Teuvo Kopra
www.teuvokopra.fi
Suomi            Tanzania

Agnes Mwandembo:

Ambonisye Mwandembo:

Agnes Mwandembo:

KANISA NA UKIMWI

 

SEHEMU YA NNE

 

MAMBO YANAYOCHANGIA KUENEA KWA VVU NA UKIMWI.

Kuna mambo mengi yanayochangia kuenea kwa VVU na UKIMWI hapa Africa. Kati ya hayo yaliyo makuu ni:-

1. Umaskini.

Wanawake wengi hufanya kazi ya umalaya kama kazi ya kumpatia kipato. Hufanya hivyo ili kumwezesha kuishi na kupata mahitaji yake ya kila siku pamoja na familia. Jambo ambalo linampelekea hatima ya yote kupata maambukizi ya VVU. Aidha vijana wa kiume na wa kike pia wanajikuta wakijiingiza katika mambo hayo, kwa kusudi la kupata fedha, chakula au mavazi kwa ajili ya kumudu maisha au starehe zao.

Kwa ajili ya hali ya umaskini, hata wanapokuwa wameathirika, huwa wanakufa haraka kwa ajili ya kukosa chakula bora na cha kutosha, pia mavazi, malazi na matibabu. Wenye uwezo wanaweza kupata dawa na chakula bora au matunzo mazuri, hivyo huwasaidia kurefusha maisha yao. Kanisa ni lazima lijitahidi kubuni njia za kuondoa umaskini, hii itasaidia kupunguza kasi ya kuenea kwa VVU na UKIMWI.

Umaskini nini?

Ni hali ya maisha ya njaa, kukosa malazi, kuumwa na kukosa matibabu au uwezo wa kuonana na daktari, kukosa shule inayopelekea kushindwa kujua kusoma na kuandika, kukosa kazi ya kujipatia kipato, hofu ya maisha, maisha ya kuishi leo tu bila akiba ya kesho, kukosa uwezo na uhuru binafsi.

Sababu zinazosababisha umaskini.

Umaskini unaweza kusababishwa na mambo yafuatayo:-

- Uvivu. (MIT. 6:9-11, 10:4, 14:23, 20:4, 4:13).

- Kuwa na pupu ya maisha. (MIT. 21:5).

- Kuwa mpuuzi. (MIT. 28:19).

- Husuda. (MIT. 28:22).

- Kupenda anasa. (MIT. 21:17, 23:20,21).

Mungu ana mtazamo gani kwa maskini?

Biblia inatuonyesha jinsi Mungu anvyoona umuhimu wa kuwasaidia maskini. (MIT. 31:8,9, LAW. 19:9-10, 23:22, KUT. 23:10-11). Mungu anawatetea maskini na wanyonge. (ZAB. 12:5). Akionyesha kuwa Bwana ndiye kimbilio lao. (ZAB. 14:6, 35:10, 82:2-4, ISA. 25:4). Yeye ana uwezo wa kuwapa chakula. (ZAB. 132:15, 68:9-10).

Mungu hapendezwi na tabia ya kumwonea maskini, (MIT. 22:16, 21:13). Mungu amewaumba wote matajiri na maskini (MIT. 22:2, 29:13, ISA. 19:22, 30:26, 45:7, HOS. 6:1-2) na amewaumba hawa wote kwa kusudi lake. (1SAM. 2:6-7).

Mungu ameahidi thawabu njema kwa wote wenye moyo mwema katika kuwasaidia maskini, na ya kuwa kwa kufanya hivyo wanamfanyia Mungu mwenyewe. (MIT. 15:31, 17:5, KUM. 15:10, MIT. 19:17, 22:9, 28:27, 11:24, 29:7, 14:21, YER. 22:15,16).

Yesu anasema, “Roho wa Bwana yu juu yangu; kwa maana amenipaka mafuta kuwahubiri maskini habari njema” (LK. 4:19, 7:22, MT. 11:5, ISA. 61:1). Hivyo maskini wanahitaji habari njema toka kwako.

Mungu anawataka watu wake kuwa na tabia kama yake ya kuwahurumia na kutoa msaada kwa wenye shida, na mahitaji mbalimbali kwa moyo na upendo wa kimungu. (2KOR. 9:7). Hutakiwi kuwatendea mambo kwa nia ya kujionyesha mbele za watu; hutakuwa na thawabu yoyote kwa Bwana. (MT. 6:1).

Unatakiwa kutoa kwa maskini na wahitaji kutokana na kile ulichonacho na wala sio usichonacho au kwenda kukopa na kuwa na madeni, na manun’guniko tele nk. (2KOR. 8:12). Ni wazi sio rahisi kutatua matatizo yote yanayowapata watu hapa duniani, au katika eneo unaloishi, lakini, unaweza kufanya kitu kwa aili yao kwa utukufu wa Mungu. (GAL. 2:10).

Fanya unachoweza kwa kutumia ulichonacho pale mahali ulipo”.

Tunajifunza kuwa Petro na Yohana walipomuona yule kiwete pale lango kuu na kujua ni mhitaji: Wakamwambia, “Sisi hatuna fedha wala dhahabu, lakini tulicho nacho ndicho tukupacho…” (MDO. 3:2-6). Wakampa, akasaidika, mhitaji akafurahi kwa shangwe kubwa, maana shida ya uwete sasa imemtoka iliyokuwa inamfanya maskini.

Mkristo anacho kitu fulani ambacho angeweza kumpa mwingine, inaweza kuwa neno la imani, tumaini, na upendo au vitu. Mambo hayo yakamfaa mhitaji au maskini. Tukumbuke tunapowatendea hao wahitaji na maskini, tunamfanyia Yesu Kristo mwenyewe. (MT. 25:31-46).

Pamoja na kuwasaidia hao, bado yatupasa kubuni zaidi njia ya kuendelea kupunguza au kuondoa tatizo la umaskini katika jamaa tuliopo, kwa kuwa ndiyo moja ya sababu kubwa za kuenea kwa VVU na UKIMWI.

2. Wanaume wanavyowaona wanawake.

Mara nyingi katika jamaa mbalimbali mwanamke amewekwa kama chombo cha kufanyia au kutimiza haja au matakwa ya mwanaume katika tendo la ndoa. Hata kama mwanaume ana tabia mbaya ya kutoka nje ya ndoa. Kama mwanamke akidiliki kukataa, basi, hulazimishwa kwa nguvu katika kushirikiana naye.

Katika baadhi ya mila, jamii ya wanaume, wanayo ruhusa ya kuoa wanawake zaidi ya mmoja au pia kurithi mke wa nduguye aliyefariki. Hali hii inachangia kuenea kwa VVU na UKIMWI. Mara nyingine majukumu ya wanawake katika mila zingine, yanawapelekea kujiingiza kwenye umalaya.

Wengi wao kutokana na maisha magumu, wanawajibika kufanya biashara za kusafiri na kwenda mbali na familia zao. Wanapokuwa huko safarini wanaingia kwenye uhitaji, aidha wa kukosa chakula, mahali pa kulala au kuhitaji msaada mwingine wa kibiashara au kusaidiwa kazi nzito inayomshinda, hivyo ili afanikishe hitaji lake anajikuta anautoa mwili wake kwa zinaa.

3. Kazi au Ajira za mbali na nyumbani. (Migration labour practices)

Kutokana na kukosa ajira mara nyingine huwalazimu wanaume kuondoka katika miji au vijiji vyao na kusafiri nje ili kutafuta kazi iwe ndani au hata nje ya nchi. Wanapokuwa huko nje ya nyumbani kwao, ili kufanya kazi aidha migodini, viwandani, au kwenye mashamba, basi, familia zao hubaki peke yao. Labda wanaweza kupata nafasi mara chache kutembelea familia zao au mara moja tu kwa mwaka wakiwa likizo. Mwanaume huyu au mwanamke anapokuwa mbali na mwenzi wake, basi, anashawishika kuwa na wapenzi wengine. Jambo hili linapelekea urahisi wa mume au mke kupata maambukizi ya VVU na UKIMWI.

4. Haki ya ndoa.

Kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali, (kumudu maisha ya wokovu), mkajiane tena, shetani asije akwajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.” (1KOR. 7:2-4).

Ni wazi kuwa mume na mke kama wanandoa, wakaipoteza haki yao; heshima hii waliopewa na Mungu, juu ya tendo la ndoa, basi, tatizo kubwa litakuwa limewaingilia. Pamoja na kupeana, vitu vizuri, kusaidiana, kuhudumiana, kupendana, kuishi katika nyumba moja nk.

Bado, pasipo kushirikiana katika tendo la ndoa ni hatari, huwafanya hawa mume na mke kuwa kama ndugu wengine wowote tu wanaoishi nao, yaani, dada, kaka, watoto, na jamaa nyingine iliyopo. Madhara yake tunaona huwa makubwa na haya ufa huanza taratibu. Upendo wa kwanza na mahusiano baina yao hupungua siku kwa siku.

Hatimaye hamu ya kutafuta mpenzi mwingine atakayekidhi haja hiyo huingia, na hivyo, kusababisha mume au mke kutenda tendo hilo nje ya ndoa yake. Ni kweli, huduma zingine anaweza kuzipata nje ya ndoa yake, kama vile, chakula – ataweza kula hotelini. Nguo - zikafuliwa na dobi, usafi - ukafanywa na msichana wa kazi nk. Lakini tendo la ndoa ni haki pekee ya wanandoa, yaani, mume na mke wake. Na kufanya kinyume cha hayo ni kuasi agizo la Mungu.

Kwa nini mume au mke anaweza kwenda nje ya ndoa?

Sababu zinawe kuwa kama maandiko yanavyoeleza ya kuwa:-

- Kunyimana

- Kuwa na amri juu ya mwili wake (matakwa yake binafsi, bila ya kujali mwenzake)

- Tamaa mbaya.

Hayo ni mambo ambayo Biblia imeyaainisha. Na hayo huweza kusababishwa na mmoja wao katika ndoa aidha mume au mke. Wanawake wengi hupenda kutumia kutoa adhabu kwa waume zao kwa kumnyima tendo la ndoa (moyoni anasema tutaonana kitandani! Utakoma ubishi!), hasa inatokea mara anapojisikia kukwazika na kuona hawezi kumsamehe kabisa, basi, anaona njia pekee ni kufanya hivyo.

Kwa ujinga huo kusababisha mwenzi wake kujaribiwa na wapenzi wengine wanaoonekana kuwa kumpenda na kumhudumia vizuri. Biblia inasema, “Mungu ameumba jambo jipya duniani, mke atamlinda mwanamume.” (YER. 31:22). Ataweza kumlinda hasa mumewe? Jambo kuu ni yeye kuona anampa haki yake inavyostahili.

Vivyo Wanaume wengi kwa kutokuonekana muda mwingi mbele za wake zao kwa visingizio vya shughuli nyingi nk, hutoa nafasi kwa wanawake kushawishika na waume wengine ili kushiriki tendo hilo. Wazo lao, huenda linawajia kuwa nitafanya mara moja tu kwa leo, na maadamu mume au mke wangu asijue.

Lakini kwa kujaribu kufanya hivyo, mara, anajikuta anajikuta ameanguka na kuvunja uhusiano wake na Mungu, uovu umeingia na kummiliki. Na hatimaye wanandoa wenyewe hujikuta kudhoofika kiimani, na mahusiano yao binasi. Pia ni hatari kubwa kwa maambukizi ya VVU na IKIMWI kwa jamaa, na kuleta shida kubwa kwa familia na watu wengine.

Kwa hiyo wanandoa wanashauriwa kuhakikisha kuwa hawanyimani tendo la ndoa kwa visingizio viwavyo vyote, kama, makwazo, chuki, kukosa vitu, kinyongo na mengineyo yasiyo ya lazima, kama vile, mwanamke kuwa katika siku zake (LAW. 15:19,25), magonjwa nk.

Kwa kuweza kutimiza haki ya ndoa, kwa kufanya bidii kila mmoja ili kuona mwenzi wake anamwonyesha upendo na kumshawishi kushirikiana naye kindoa kwa kadiri awezavyo; ni kweli kabisa, tutaponya ndoa zetu na pia kuepukana na vishawishi vya nje viletavyo pia maambukizi ya VVU na UKIMWI na hatimaye kuleta majonzi kwa wanandoa.

Mungu akubarikie!


WebDesign Miia Metsola